Monday, June 18, 2012

Sebastian Maganga: Bajeti 2012/13-wali maharage shilingi 100,000 kwa sahani.



Mambo vipi? Naitwa sebastian maganga, mdau wa masuala ya redio za burudani na meneja wa vipindi cloudsfm,

Nataka upige picha hii kwenye fikra zako, baada ya pilika za asubuhi, mchana unakuja na hisia ya njaa inakuvamia  hivyo unaamua kwenda kwenye kijiwe chako cha kawaida cha mama lishe, unapofika tu unakutana na bango kubwaa, linalosoma maneno haya “wali maharage..ni shilingi 100,000  kwa sahani” katika hali ya kawaida utajikuta uko kwenye mshangao, pili utamfuata mama lishe huyo na kuhoji chanzo cha kufumuka huko kwa bei kutoka shilingi 600 hadi shilingi 100,000 yeye anakutaarifu kuwa vitu vimepanda beiii, unaona kabisa maelezo hayo hayajitoshelezi na unaendelea kudadisi kuhusu mfumuko huo mkubwa wa vitu ambavyo kwa mantiki ya kawaida kabisa vinatakiwa kuuzwa kwa bei ya chini zaidi ya hapo, iweje? Wali maharage yanayouzwa shilingi 600 kwa sahani yapande bei mpaka shilingi 100,000? Kwa siku moja tu? Katika mazingira yale-yale? Bila maboresho au chochote kinachoashiriwa mabadiliko makubwa ya uwekezaji yenye thamani hiyo? Ghafla unashtuka kutoka usingizini na unashukuru mungu kuwa ile ilikuwa ni ndoto tu!!!!

Japokuwa itachukua miaka mingi saana mpaka “mama ntilie” atafikia hatua ya kuuza sahani moja ya wali maharage kwa shilingi 100,000 lakini suala moja muhimu linabaki , wewe umeelewa vyema hadithi ya ndoto husika, kwani vihusishi vingi katika ndoto ile vinazunguka maisha yako ya kila siku.

Tuchukue mfano huu katika mazingira yafuatayo, tunataka kutoa maelezo ya namna ambavyo bajeti ya serikali itaathiri maisha ya kawaida ya mtanzania, kwa njia ambayo itaeleweka zaidi kwake na mazingira yake,  kosa ambalo mara nyingi tunalifanya ni kuwatafuta wataalamu wa masuala ya kifedha, kiuchumi na pengine kisiasa ambao hupewa fursa ya kutoa maelezo ya kuhusu faida na upungufu wa bajeti husika, lakini unakuta baada ya kufanya hivyo wananchi au waskilizaji wanatoka kapa, kwanini? Jibu ni jepesi...kwasababu mtaalamu asipoambiwa na wahusika wa kituo kuhusu njia ya kutoa maelezo yake, atabaki kutoa maelezo ya kitaalamu kana kwamba anaongea na wataalamu wenzie na wasomi, na si watu wa kawaida ambao hawana elimu wala ufahamu wa kina wa masuala ya uhasibu, fedha au uchumi.

Ndugu mtayarishaji au mtangazaji wa redio cha kufanya ni  kumweleza huyo mtaalamu kuwa achukue mifano ya vitu vya kawaida vinavyowazunguka wananchi wa kawaida, na baada ya hapo sasa anapotoa hoja  kuwa bajeti ya mwaka huu haitoi nafuu kwa maisha ya kawaida ya mtanzania ahusishe mifano yenye kujenga taswira inayoeleweka, kwa mfano jinsi ambavyo mtanzania wa kawaida atalazimika kulipa shilingi kadhaa kwa sahani ya wali maharage badala ya shilingi kadhaa ambazo alikuwa anazilipia awali kisha baada ya hapo achanganue kwanini hayo mabadiliko yatakuwepo.

Kufaulu kwa matangazo yetu ya redio kunategemea sana mawasiliano ambayo yataeleweka vyema na wasikilizaji kuliko kuleta tu jopo la watalaamu ambao wataishia kuonekana mahiri kwa wataalamu wenzao, na kuwaacha waskilizaji wengine gizani...karibu lanchi (wali maharage kama kawa!!!)


No comments:

Post a Comment