Dr. Ulimboka |
Kituo cha ITV kupitia Twitter kimesema mwenyekiti wa jumuiya ya madakatari Dr. Stephen Ulimboka ametekwa na kupigwa na watu wasiojulikana na anapelekwa katika hospitali ya mifupa ya Moi.
Kwa mujibu wa mtandao wa Jamii Forums Dr. Ulimboka ametekwa majira ya saa sita usiku na watu watatu waliokuwa na silaha za moto na kumpeleka kusikojulikana! Inasemekana alipigiwa simu na jamaa mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la 'Abeid' ambaye tangu mwanzo amekuwa akiwasiliana naye na kujiita afisa wa serikali na kudai kuwa alitaka aonane naye face to face kwa ajili ya mazungumzo.
Tukio hilo limetokea wakati kumekuwepo na mgomo wa madaktari nchi nzima ambao hata hivyo wameonekana kusalitiana kwa kutokuwa na msimamo wa pamoja, kwani maeneo mengine yote huduma zimeendelea kama kawaida, isipokuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Madaktari hao wametangaza mgomo usio na kikomo kwa lengo la kuishinikiza serikali kutimiza mahitaji yao, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kuwapandishia mishahara.
Licha ya mgomo huo kuanza kuleta madhara kwa wagonjwa katika siku ya kwanza juzi, kwa madaktari kutofanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini, jana hali hiyo ilikuwa tofauti kwani sehemu nyingi huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.
Kwa upande wake mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amesema amesikitishwa sana na tukio hilo na serikali inapaswa kuwajibika kuwaeleza wananchi.
‘Kaka Zitto,hali ya Dr.Ulimboka yuko unconscious,multiple ribs fracture na kwenye mikono pia amevunjika pamoja na taya,yuko icu wanamstabilise kwanza kwasababu hapumui vizuri,the situation here is really bad,I agree with you this is outright outrageous’
Nimechukizwa sana na habari za kutekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya kwa Dr Ulimboka, Kiongozi wa Madaktari Nchini. Mambo kama haya tumezoea kuyasikia kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kiimla ambapo watawala badala ya kutumia njia ya kidemokrasia na kisheria kushughulikia wanaoamini ni maadui zao katika utawala, hutumia wahuni katika Taasisi za usalama kuteka raia, kuwatesa, kuwafunga na hata kuwaua.
Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko. Nimezungumza na baadhi ya madaktari walio karibu na Dokta Ulimboka na kujulishwa kwamba majeruhi huyu wa vitendo vya hovyo kabisa kutokea hapa nchini alikamatwa jana usiku mnamo saa sita na watu wasiojulikana na kupelekwa katika msitu wa MagwePande na kujeruhiwa vibaya. Habari hizi bado hazijathibitishwa na vyanzo huru lakini ndio zilizopo hadi hivi sasa.
Serikali kama mlinzi wa usalama kwa raia inaWAJIBU kueleza tena kwa haraka ni nini kimetokea kwa kijana huyu msomi na kiongozi wa wataalamu wenzake. Serikali INAWAJIBIKA kueleza katika nyakati kama hizi ambapo kuna mgogoro kati yake na madaktari imekuwa wapi kuhakikisha usalama wa viongozi wa madaktari ili kuepusha watu wanaoitwa ‘agente provocateure‘ kuweza kuhatarisha hali ya amani ya nchi na hata kupelekea kuweka hali ya vitisho kwa madaktari wetu.
Serikali INAWAJIBIKA kueleza kama sasa imeamua kutumia njia za kihuni kumaliza matatizo na wananchi wake.
Nimemuomba Waziri kivuli wa Afya wa CHADEMA kufuatilia suala hili kwa kwa karibu sana ili kuhakikisha kwamba ukweli wote na ukweli mtupu unafahamika. Kamwe hatuwezi kuacha Mtanzania yeyote aonewe, anyanyaswe au akandamizwe eti kwa sababu ya kudai haki yake na za wenzake. ‘An injury to one, injuries to all’
Naomba madaktari wamwangalie kwa karibu daktari mwenzao ili aweze kupata nafuu. Ulinzi uimarishwe ili kuhakikisha usalama wake.
No comments:
Post a Comment