Ijumaa ya leo June 29 ndio siku ambayo Season One ya ‘The Music Postmortem inaanza rasmi hapa leotainment. TMP itakuwa inakujia kila ijumaa pale ambapo tutakuwa tumepata mezani wimbo mpya unaostahili kufanyiwa uchambuzi wa muziki na wataaalam wa mambo hayo.
Katika msimu huu panel ya wachambuzi wa TMP ni pamoja na Wynjones Kinye (mtunzi wa nyimbo, muimbaji, producer na Tutorial Assistant, St. Augustine University of Tanzania, Fredrick Max ( Banker, msomi wa masuala ya biashara, IFM na mtunzi wa nyimbo, Joseph 'Josefly' Muhozi (Rapper, mtunzi wa nyimbo, mtangazaji wa radio, mwanafunzi wa Mass Communication, SAUT, na Jeremy J-Ryder Kyejo (producer Tongwe Records na msomi wa masuala ya muziki).
Wiki hii magwiji hawa wa muziki nchini wanauchambua wimbo wa Belle 9 na Ben Pol uitwao ‘Anayeishi Naye. Wimbo huu umetengeneza na producer Mona G.
Wynjones Kinye
Iko wazi kwamba hawa mabwana wawili wanasauti nzuri na za kipekee…ni aina ya waimbaji ambao Tanzania majina yao ni rahisi sana kutajwa vinywani mwa watu pindi wazungumziwapo waimbaji wakali.
Sijasikia wao kustruggle kuhit high notes za chini, kati, na juu….wamepokena vizuri na hii inadhihirisha kuwa walikaa pamoja kutunga ama kuupractice wimbo kitu ambacho waimbaji wengi wa Kitanzania hawafanyi pindi wakishirikiana kwenye wimbo.
Nimependa wao kupokeana kuimba ndani ya ubeti na kiitiko….hii imefanya wimbo usiwe rahisi kuchokwa, utundu wa kila mmoja kucheza na sauti umenogesha zaidi mtindo walioamua kuutumia.
Uhusiano wa ujumbe na muziki uliotengenezwa sio mbaya…tempo iko sawa na waimbaji wamehakikisha wanatamka maneno vizuri kufikisha ujumbe kusudiwa….lakini niseme production kwa kiasi kikubwa sana inachangia wimbo kuwa mahala pazuri sokoni…siwezi sema kwamba hii ni production bora kabisa kuustahili wimbo huu …najaribu tu kujikumbusha kuwa huku ndipo alipoanzia Belle ambaye baadae alipanda ngazi nyingi sana na leo amefanya maamuzi magumu ya kuamua kushuka ngazi kurudi kufanya wimbo huu ambao wengi wangetegemea uwe collable ya mwaka.
Nachojaribu kuwasilisha hapa ni kuwa tumeshamsikia sana Belle kwenye midundo ya aina hii…binafsi nilitamani mdundo wa tofauti kabisa na wenye ubora wa hali ya juu kwa vijana.
Adlibs za Belle zimependezesha sana nyimbo…amejikamua vizuri mno kutamka “no no no nooo” …wapenzi wa Wyclef Jean watakuwa wameenjoy sana ladha ile japo sauti hizo kusikika wakati chorus inaimbwa kwangu mimi haikuwa sehemu muafaka.
Title…hapa wengi tunakwama mpaka wakati mwingine hadhira kubatiza jina jipya wimbo Fulani…katika wimbo huu naona dalili zote za hili kutokea….Kama ingekuwa ni mimi wimbo huu ningeuita “AMETUDANGANYA” badala la “ANAISHI NAYE”…sababu ni rahisi tu kwamba wimbo huu hapa ndipo panabamba kirahisi na kumfanya mtu kuitikia..lakini pia content imeegemea zaidi kwenye namna alivyowadanganya kuliko kuishi naye.
Nimefurahia zaidi uamuzi wa Belle kutorudiarudia vipande vya mistari kwenye beti kama alivyofanya kwenye nyimbo zake nyingi….hii imefanya midondoko yake isiwe “predictable” kitu ambacho ni kizuri masikioni mwa msikilizaji.
Uhusiano wa title na content: Uhusiano kati ya jina la wimbo na content hapa haupo…hivyo siwezi sema kwamba kiuandishi wamefanikiwa sana…japo haimaanishi kuwa wimbo ni mbaya...nilitamani sana kusikia namna mtunzi angeweza kuunganisha jina la wimbo na ujumbe aliouandika ndani.
Fredrick ‘Mshale’ Max
Ben pol and Belle 9, nani asiyewajua wakali hawa kwenye tasnia ya muziki wa Bongo? Ni dhahiri isiyojificha kwamba hawa jamaa ni wakali wa vocals na wamejizolea mashabiki lukuki kutokana na nyimbo zao kali.
ANAISHI NAE ndio jina la single yao mpya kama collabo. Kwakweli wengi tuliisubiri kwa hamu,ukizingitia vipaji walivyo navyo vijana hawa. Well ,I must say I am very disappointed in their failed attempt to create a masterpiece...nyimbo hii INAONEKANA WALIKURUPUKA....beat ni mediocre, nothing special about the beat kwa kweli...lyrics hafifu..hazijaendana na uzito wa idea kabisa...Melodies Mbaya...ukiacha kipande cha Anayeishi Nae....wanapoitikia..arrangement mbovu.
The only good thing about the song ni vocals za wasanii.
Hata hivyo, jitihada za belle 9 kuweka ad libs zimefail...mwishoni anapayuka badala ya kuimba..and Ben pol..whistle notes Mwachie Mariah Carey...hazikutoka poa.
All in All ni Generic song,ya kawaida sana..I give it 2 stars out of 5.Vijana Wajaribu tena...and the producer...what is his name again? needs to take a seat at the National Stadium.
And a message to all Bongo artists, just because you like each other’s music doesn't, mean you can create magic together, there’s gotta be some chemistry.
Joseph 'Josefly' Muhozi
Mwanzo(Introduction) umepangwa vizuri na unavuta sana usikivu, mwanzo mfupi wa kuvuta hisia tu..ama (feeling) kama inavyojulikana kwa lugha ya studio..
Kizuri zaidi ni pale walipounganisha na kibwagizo(chorus) ambayo inatoa picha ya ujumla ya kisa kizima kwa ufupi, na majina yao kwa utangulizi ambayo yakitajwa kwa pamoja hapana shaka msikilizaji atatamani kujua nani kafanya nini kwani hawa wote ni wakali. Maneno machache ya chorus na mepesi kueleweka yanayotoa picha ya ujumla ya simulizi tena bila mdundo yakisindikizwa na kinanda..
Ubeti wa kwanza umeanza vizuri kwa misemo ya Kiswahili inayotoa picha ya mtu anaelalamika, belle 9 anasema ‘’kweli furaha au matatizo huja wakati usiodhani, kwani ndivyo imekua sivyo alivyofanya mi siamini’’..lakini pia wanavyodakizana Ben Paul na Belle 9 kwa mistari miwili miwili kila mmoja akieleza matumaini yake na jinsi yalivyopotea (kwa kutumia mistari miwili miwili tu (mirefu na sio mifupi))..na kuunganisha kisa hiki kinachovutia kwa mstari mmoja mmoja kuonesha jinsi gani kila mmoja alikua hajui kama ahadi alizopewa na Yule mrembo zilikua ‘copy’ ya zile alizopewa rafiki yake..
Kwa huu ubeti wa kwanza tu..mtunzi/watunzi wamefanikiwa kufanya kile wataalamu wa mawasiliano wanakiita ‘’teasing the audience’’ japo kwa ukawaida neno hili linaweza kua na maana nyingine lakini kwa taaluma ya mawasiliano ya umma inamaanisha kumfanya msikilizaji kua na shauku ya kujua nini kilitokea, na hapo inabidi sasa asubiri ubeti wa pili..wakati ameshapata picha zaidi ya kisa kizima ila anahitaji kujua tu ilikuajekuaje ‘HOW’....
Baada ya chorus..Ubeti wa pili..ambapo wameweza pia kutoa kile ambacho msikilizaji alitaka kujua baada ya kusikiliza ubeti wa kwanza.. ‘HOW’ ilikuaje kuaje hawa marafiki wakajikuta katika huu mtego wa huyu binti..na katika ubeti huu wameweza kueleza ilikuaje, na hapa wametumia ubuinifu kwa kukumbushana matukio muhimu kwa kusimuliana wao wenyewe na kutoa picha ‘inayotatanisha’ kidogo kwa jinsi walivyoonana na mmoja akiwa na huyo huyo msichana, na hawakusalimiana...nitaitolea ufafanuzi hapo chini..
Mwisho kabisa mtunzi ameweza kwa kiasi kikubwa kusimulia na kutoa kisa kizima kisichohitaji muendelezo kwa sababu inaonekana kabisa kua Yule mrembo alishapata mtu mwingine ambae amepiga nae hatua kubwa zaidi ya zile walizopiga wote kwa sababu huyo jamaa‘‘ANAISHI NAE’’.
Na wao wamebaki na ‘MAJUTO’ tu, ambayo kwa msemo wa Kiswahili ‘NI MJUKUU’.
CHANGAMOTO: nimejaribu kufanya sampling ya kutaka kujua uelewa wa watu 5, na wanne kati yao wameweza kupata mkanganyiko hasa kwa imagination kutengeneza picha ya hiki kisa katika hii mistari ya ubeti wa pili..na mmoja kati yao alipata picha ambayo ni sahihi...
BEN PAUL: Siku ile mlipita we ukiwa nae, hamkuniona nilisimama kando asijue
BELLE9 : Mbona mi siku ile nilikuona, sikujua kama Yule mmnajuana
BEN PAUL:Kitambo mi nilimshindwa sikujua kama unampenda
Nilijua penzi atalitunza sikujua kama angetuchanganya
Wanne walisema Ben Paul aliwahi kumuona Belle 9 na huyo msichana, na pia Belle 9 katika siku nyingine aliwahi kumuona Ben Paul na msichana huyo huyo..
Lakini hapa ni kwamba wakati Ben Paul anawaona Belle 9 na Yule msichana, akajificha ili Yule msichana asimuone kwa sababu alikua ameshaachana nae na alishangaa kumuona na Belle 9 ambae ni rafiki yake...kumbe hata Belle 9 Nae alimuona ila hakutaka kumuita na hakujua kama Ben Paul pia anamjua huyo msichana, nadhani ni sababu pia Ben Paul alijificha na unajua tena mtu ukiwa na motto wa kike huwezi ku-shout kumuita mshikaji...hahahahaa....na huu ndio UTUNZI mzuri wa simulizi..unatengeneza picha zinazokubali katika uhalisia.
Mwisho kabisa natofautiana na wale wanaodai kua wimbo huu unafanana na SAME GIRL wa R.KELLY& USHER...ni tofauti kabisa..labda mfanano ni kwa sababu wanaongelea msichana mmoja...ila simulizi ni tofauti kabisa.. kwa wimbo wa kudakizana na simulizi huu pia ni moja ya nzuri kiutunzi zilizowahi kusikika kwa kudakizana kwa Tanzania..
Jeremy J-Ryder Kyejo
First impression, ukisikiliza beat ina melody poa sana, rhodes instrument mona gangster aliyoitumia pia iko freshii.
Mixing
Mixing ya beat inaweza kuwa nzuri zaidi, mfano hats zile kuwa panned more left na right, kama kwenye mfumo wa live drums na pia cutting frequencies kwenye hats ambazo zina interfere with other sounds, for instance cutting frequencies less than 600hz, using a highpass filter. Kwa Vocals..nimezipenda, ila reverb mix (amount) ingepungua kidoogo...ili iweze sit kwa mix poa zaidi.
Generally ngoma iko mzukah, collabo wamefanya poa sana.