Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu wimbo wa MwanaFA aliomshirikisha AY na Dully Sykes uitwao Ameen kwamba umesample wimbo wa Cecile uitwao Hey.
Kila mmoja anasema la kwake na Dully Sykes amesema haoni kama amefanya kitu cha ajabu. Akihojiwa na East Africa Radio, msanii na producer huyo alisema sampling ni kitu cha kawaida na watu kibao wanafanya. Japo alisahau kuwa pamoja na kwamba ni kweli watu wanarudia sana nyimbo za zamani, wasanii hao huclear kwanza masuala ya haki miliki kwa kuwalipa ama kuwaomba ruhusa wamiliki wa kazi hizo.
Alichokifanya Dully ambaye ndiye producer wa wimbo huo ni kuchukua melody na mdundo wa beat ya wimbo wa Cecile na kutengeneza version yake inayofanana na wimbo huo. Kabla ya kuangalia kama ikitokea Cecile anamshtaki Dully kesi itamwangukia nani, hebu fahamu kwanza dhana ya sampling ikoje duniani.
Katika muziki, sampling ni kitendo cha kuchukua kipande ama sample, ya sauti/wimbo uliorekodiwa zamani na kukitumia kama mdundo, beat au sauti kwenye wimbo mwingine.
Mara nyingi "samples" hujumuisha sehemu moja ya wimbo ambayo baadaye hutengenezwa kuwa beat ya wimbo mwingine.
Kwa mfano, nyimbo za hip hop zilizotengenezwa na madj kwa kurudia kipande fulani cha wimbo ili kutengeneza mdundo unaojirudia lakini ukiwa kwenye mpangalio unaoufanya uweze kuchezeka.
Matumizi ya samples yamekuwa na shida kisheria na kimuziki pia. Wahasisi wa mtindo huu miaka ya 1940s hadi 1960 nchini Marekani, wakati mwingine walikuwa hawatoi taarifa ama kuomba ruhusa kwa wamiliki halisi wa kazi hizo kabla ya kutengeneza nyimbo ama beat zilizo na sampes hizi.
Mwaka 1970s, wakati hip hop ilikuwa ikichezwa tu kwenye sherehe za mitaani hakukuwa na ulazima wa kushughulikia masuala ya haki miliki ili kusample wimbo utakaotumika kwenye sherehe hizi. Lakini baada ya kuanza kurekodi kazi hizi za rap miaka ya 1980s na baadaye kuingia kwenye mkondo mkuu wa muziki nchini Marekani kukawa na umuhimu wa kulipa kwanza ili kupata ruhusa ya kisheria kutumia samples kitu ambacho kilikuwa kigumu kwa watu wote bali kwa madj, maprodusa na rappers waliokuwa wamefanikiwa.
Matokeo yake idadi kubwa ya wasanii wakajikuta wameingia kwenye matatizo kwa kutumia samples bila kutoa credits, kuomba ruhusa ama kulipia.
Muziki wa hip hop baadaye ukahamia kwenye utaratbu kamili ambapo sampling ikawa njia mojawapo tu ya kuunda beats, huku maprodusa wengi wakaanza kutengeneza beats kwa idea zao mpya kabisa.
Licha ya matatizo ya kisheria sampling imekuwa ikisifiwa na kukoselewa pia.
Wapo wanaosema kuwa mtindo huo unaonesha namna watu walivyoishiwa na ubunifu na wengine wakidai kuwa sampling inaonesha mapinduzi ya muziki.
Wale ambao kazi zao zimefanyiwa sample nao wamekua na mtazamo tofauti ambapo wapo wanaounga mkono wengine kuponda.
Kusample bila ruhusa kunavunja sheria mbili za haki miliki. Ya kwanza ni ‘the sound recording copyright’ (inayomilikiwa na kampuni ya kurekodi) na haki miliki ya wimbo wenyewe inayomilikiwa na mwandishi mwenyewe wa wimbo ama kampuni ya uandishi.
Hivyo kama unataka kusample kihalali ni lazima upewe ruhusa kutoka kwa mmiliki wa wimbo huo. Mmiliki halali kwa upande wa sheria za wenzetu ni kampuni iliyouandika ama record label. Hivyo ni lazima upate ruhusa kutoka kwa sehemu zote mbili.
Ada ama malipo ya kutumia samples inatofautiana sana. Ada itategemea ni kiasi gani cha sample unachotaka kutumia.
Mara nyingi ada ya kutumia sample huanzia $250 hadi $10,000 kwenye label kubwa.
Hivyo kama ukutumia samples bila kuclear masuala hayo kuwa tayari kupigwa penalty. Bahati nzuri Bongo tuko mbali na muziki wetu haufiki kwa wingi nchi za watu lakini mpaka sasa ni wengi wangekuwa kwenye matatizo makubwa. Faini ya kutumia kazi ya mtu bila ruhusa huanzia $500 hadi $20,000 kwa kitendo kimoja cha kukiuka sheria za haki miliki katika muziki.
Kama mahakama ikigundua kuwa kumefanyika uvunjifu wa sheria hizo kwa makusudi faini inaweza kufikia $100,000.
Mmiliki halali wa kazi anaweza kupewa pia ruhusa ya kuzuia usambazaji wa kazi hizo ama kuziteketeza.
Dully anasimama wapi?
Kwa maelezo hayo hapo juu ikitokea Cecile ameusikia wimbo huu wa MwanaFA Basi Dully (ambaye ni producer) ajiandae kulipa kwasababu kesi hii hawezi kushinda. Pia kesi hii si ya Dully peke yake, MwanaFa naye atahusika. Hawezi kushinda kwasababu ametumia melody iliyomo kwenye wimbo wa Cecile kutengeneza beat yake bila ruhusa kutoka kwa mwenye wimbo.
Na wale wanaosema kuwa beat hiyo ni riddim kwa hiyo hakuna haja ya kupewa ruhusa wanatakiuwa wafahamu kuwa Hey ya Cecile ipo kwenye albam yake rasmi iitwayo Jamaicanization na sio Riddim. Ni wimbo wake binafsi ambao kama mtu akitaka kutumia lazima apewe ruhusa kutoka kwake.
Tunakosea tunaposema ‘sampling ni kitu cha kawaida’ bila kufahamu kwamba ukitaka kusample ni sharti upewe ruhusa, ununue na pia utoe credits. Kama Ameen ingetoka ikiwa imeambatanishwa na maelezo kuwa wimbo huu umesample ngoma ya Cecile uitwao Hey hakuna ambaye leo hii angekuwa anajadili issue hii.
Hata hivyo, kutoa credits hizo kusingemkomboa Dully kutoka kwenye uvunjaji wa sheria za haki miliki kama Cecile akitaka kufuatilia.
Tushukuru tu Mungu kuwa tupo kwenye nchi ambayo ni ngumu kwa wasanii wakubwa kusikia nyimbo zetu, lakini kama tulivyosema hapo juu ni kwamba maproducer wengi wa Tanzania leo hii wangekuwa wameshajikuta kwenye matatizo.
No comments:
Post a Comment