Friday, July 13, 2012

The Music Postmortem: Sihitaji Marafiki by Fid Q ft. Yvonne Mwale








Leo (July 13) tunauchanachana Sihitaji Marafiki wa Fid Q aliomshirikisha mwanadada wa Zambia Yvonne Mwale.

J-Ryder hakushiriki kwenye uchambuzi huu kwakuwa yeye ndiye aliyeuproduce wimbo. Tumejaribu kuwatafuta maproducer wengine wawili akiwemo Dunga na DX wa Noiz Maker kushika nafasi yake kwenye uchambuzi wa ngoma hii kwenye aspect  ya production lakini DX ameupata ujumbe kwa kuchelewa hivyo atajiunga nasi kuanzia wiki ijayo na kwa upande wa Dunga tunahisi bado hajaupata ujumbe.

Fred Max amepata udhuru naye pia hakushiriki siku ya leo. Lakini hata hivyo tumetumia uchambuzi kidogo wa msomi Evarist Chahali aliyepo masomoni nchini Scotland yaliyochambua wimbo huo. Let's Go!!

Wynjones Kinye

Nani wa kuupinga uimara wa Fareed kwenye game ya hip hop? Napenda swali hili ajibu mmoja mmoja kimya kimya!!
“Sihitaji Marafiki” muendelezo wa matoleo ya “KITAAOLOJIA” inatupa picha ya mbele ya jinsi kiu yetu itakavyokatwa….tuliielewa mitaa na sasa anatueleza mambo mazito ya kimahusiano muhimu hapa duniani!! Wapo ambao hutowaaambia kitu kwa marafiki kwa namna walivyoshibana na kutoana ktk mambo mbalimbali.

Hata mtunzi mwenyewe naamini pamoja na kutunga hivi wapo wawili watatu ambao kwake ni marafiki (kwa kupenda au kutopenda)…hivyo naweza sema kuwa Fid ni jasiri mkubwa kutunga hivi.

Nimependa title ya wimbo kwani inakushawishi kusikia vitu vilivyomo ndani…na unaposikia content mwisho wa siku utasema kweli huyu bwana anamaanisha anachosema. Kwa wafuatiliaji wazuri mtakumbuka wiki mbili zilizopita nilisema kitu kuhusu umuhimu wa title kugusa content (alichofanya Fid ndicho nilichomaanisha).

Sifa kubwa inaayomtofautisha Fid na wengine wanaofanya muziki wa aina yake (ukiacha utunzi hatari na “uvuvi” wa maneno mazuri na mazito) ni utamkaji wa maneno mengi kwenye mstari mmoja na kumudu kuingia kwenye mstari mwingine kwa kasi na wingi uleule…hili linahitaji pumzi mno…wapo ambao wanafanya hivi lakini kwa kuungaunga wakati wanaingiza vocals….si kitu kizuri kuungaunga kwakuwa ugumu huja wakati unafanya show live.

Nimesikiliza huu wimbo na sehemu moja imenikereketa, licha ya kwamba ameunga lakini pia imenipa shida kusikia neno lililoishia…sikiliza huu mstari kwenye Sekunde ya 45’…“siku hizi mabinti wananimiss ndio walionidiss uso…”
Yvonne Mwale!! Kazi nzuri toka kwa mdada huyu…simple chorus yenye wepesi wa kushikika…ni ni aina za chorus ambazo watu wanaamka nazo na kujikuta siku nzima wanazirudiarudia…wale ambao yamewakuta wananielewa zaidi nachomaanisha.

Josefly

Mi nitaendelea kuwa katika upande wa mashairi, na nitamtaja “Fid Q” kama mtunzi ili nisilirudierudie hili jina.
Kiufupi huu wimbo ni wimbo ambao umebeba mashairi mazito sana kiutunzi, na naweza kusema kuwa huu ni utunzi ambao utaufanya wimbo uwe na maisha marefu sana hata baada ya muda wa kupigwa redioni. Ukiachana na instrumental na mtindo mzuri wa kughani, mashairi yamebalance kabisa uzito wa jina la Mtunzi.

Kuanzia jina la wimbo, negative title inayovuta udadisi wa msikilizaji kutaka kujua kwa nini mtunzi ameamua kuwa tofauti kabisa na kile jamii imekua ikikipigania na kukisifia ili kuleta umoja, tunajua wapo wanaosema “utajiri wa kwanza ni kua na marafiki”, na hata wasanii wengi wanapohojiwa husema mafanikio ya kwanza aliyoyapata ni kuwa na marafiki wengi..sasa inakuwa vipi huyu jamaa hahitaji marafiki!!!! Na hapo ndipo sanaa ya wimbo huu ilipoanzia na kufaulu kwa kiasi kikubwa.

Tukizama kwenye beti tatu za huu wimbo,lazima utakubali kabisa kuwa mashairi haya yametungwa na mtu mwenye upeo mkubwa sana, na uwezo mkubwa wa kufikiri..Content imeweza kugeuza ile negative title na kumfanya msikilizaji kuwa na mtazamo chanya kuhusu jina la wimbo “sihitaji marafiki.” Na hii ni kwa sababu mtunzi ametoa sababu za msingi na anaongea kutokana na experience yake na urafiki..

Ukiacha punch lines zilizotumika ambazo ni karibia kila mstari, kuna metaphor zilizotumika ambazo zimeleta picha nzuri na zinaweza kukaa katika akili ya msikilizaji na kuunganisha mwenyewe..mfano “masaa hayarudi nyuma kama muda wa kufuturu.”

Pia ameweza kumshirikisha msikilizaji kwa kiasi kikubwa sana katika huu wimbo kwa kumuuliza maswali kama  “rafiki wa kweli yukoje.. ni mkimya au anayechonga/yule aliyekupa jina?au pengine anayekuponda? anayezuia usidondoke au  anayesubiria kukuokota?/au ni yule ambaye ukimuudhi anakutusi kabla hajaondoka?

Hii nimeipenda sana pia…na pia nimegungua hata ushauri wake kwa msikilizaji umekua ni mstari ambao wengi wameupenda na kuushare kwenye facebook page zao, inaonesha kua mtunzi ameweza kuwashawishi kwa kiasi kikubwa “hakuna adui mbaya kama rafiki yako mwenyewe, ambaye hajui ka yupo nawe.. au yupo kinyume na wewe/bora adui.”

Changamoto: Utunzi wa aina hii umeyaacha maneno ambayo ni tata huenda wengi wasiyaelewe kabisa..kama “sihitaji marafiki, labda baadaye wakitokea/aje mmoja wa kuongea nae, na mwingine wa kumuongelea” hapa kila mmoja ataelewa kivyake..wa kuongea nae, na wakumuongelea kivipi..kumuongelea on behalf of.., au kuongea kuhusu mambo yake,..na kwa kua ndo msitari ulioleta conclusion ya wimbo..coz ndiye rafiki ambae  FID Q anamuhitaji... na pia lugha ya kiingereza aliyochanganya inaweza isieleweke sana kwa watu wengi..

Dah, kwa ufupi, hii tungo ni moja kati ya tungo za kukuna kichwa sana..ambazo ndizo zinastahili kupewa heshima sana..

Evarist Chahali

SITAKI MARAFIKI haimaanishi marafiki si muhimu bali kwa kutumia kipaji chake kikubwa cha kuwasilisha ujumbe kwa namna inayohitaji tafakuri, Fid anaweka wazi mtazamo wake kuhusu mahusiano katika jamii,kwa kutumia mfano mwafaka wa marafiki.

Nadhani ushaskia msemo  'MARAFIKI WA NINI KAMA MAADUI WANANISAIDIA.' Mara nyingi,marafiki zetu hupenda kututendea mazuri tu tunayotarajia kutoka kwao na pengine kuepuka kutueleza 'hapa umechemka.'

Lakini maadui zetu huwa mahiri wa kuonyesha kasoro zetu (hata kama ni kwa uchache) japo kimsingi matarajio yao huwa ni kuonyesha mabaya yetu.

Kwa hiyo pasipo kukusudia,maadui zetu wanaweza kuwa na mchango fulani chanya katika maisha yetu kwa sababu hawana unafiki katika kunyooshea akidole mapungufu yetu.

No comments:

Post a Comment