Friday, August 17, 2012

TBC yawaomba radhi waislam kwa kutoa takwimu zisizo sahihi

Mkurugenzi Mkuu wa TBC Clement Mshana

Shirika la utangazaji Tanzania, TBC, leo limewaomba radhi waislam nchini kwa kutoa takwimu zisizo sahihi za waislam na wakristu.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Clement Mshana amefafanua kupitia kipindi cha Jambo Tanzania leo asubuhi kwa kukiri kuwa mmoja wa watangazaji wa TBC1 alitaja takwimu za  wakristu kuwa ni asilimia 52% na waislam asilimia 32% zilizopatikana kutoka mtandao wa Wikipedia.

TBC imeomba radhi kwa kuwapotosha watanzania kwakuwa takwimu hizo sio sahihi.

Mshana alikiri kuwa TBC ilifanya kosa kuunukuu mtandao wa Wikipedia na kudai kuwa chombo chenye mamlaka na cha kuaminika ni  Wakala wa Takwimu nchini na sio wikipedia.

Mkurugenzi huyo amesema tarehe 15, May, 2012 shirika hilo liliandika barua ya kuomba radhi kwa jumuiya ya waislamu nchini na kumpa onyo mtangazaji aliyetaja takwimu hizo.

Ametaka waislam kusahau yaliyopita na kuutumia mwezi huu wa Ramadhan kusamehe huku akiwataka wananchi kujitokeza zaidi kwenye zoezi la sensa litakalosaidia kupatikana kwa takwimu sahihi.

No comments:

Post a Comment