Saturday, July 7, 2012

Maajabu: Hela za sadaka zageuka makaratasi





Wanasema maajabu kamwe hayataisha. Huko Nigeria kwenye parokia ya St. Mary's mjini Jos, Plateau State, wameshangazwa baada ya kupotea kimauzauza naira 300,000 (sawa na karibu shilingi milioni 3) zilizobadilika kimaajabu na kuwa makaratasi.

Vyanzo vya nchini Nigeria vimedai kuwa tukio hilo la ajabu limetokea kwenye benki ya  Zenith tawi la Jos, ambapo katibu wa kanisa Miss Ifeoma Eze alikuwa ameenda kuziweka benki fedha hizo za sadaka kwa siku hiyo.

Ifeoma alieleza kuwa pesa hizo zilikuwa salama alipoondoka nyumbani kuelekea benki lakini alipofika kwenye kaunta ya benki hiyo hakuelewa ni kwa namna gani fedha hizo ziligeuka na kuwa vipande vya karatasi alipofungua mfuko alimokuwa ameziweka.

Alichanganyiwa na kuogopa kiasi cha kumfanya aanze kupiga mayowe (kama wale wanawake kwenye movie za kinaijeria) ambapo wateja wengine walimzunguka kumuuliza kunani!

Miss Ifeoma alisema alikuwa amechanganyikiwa zaidi kwakuwa alijiuliza angemweleza nini padre aliyemkabidhi fedha hizo!

"Ni habari ambayo inakuwa vigumu kumweleza mtu sababu wengi hawataanini,” alisema.

Kudhihirisha kuwa alichukua fedha za kweli kwenda benkini hapo, Miss Ifeoma alisema kwanza alibadilisha chenchi ndogo ndogo na kuchukua kubwa ili kurahisisha uwekaji.

Ingawa waamini wa kanisa hilo wanahisi kuna mchezo mchafu umefanyika, Askofu wa parokia hiyo Father Emmanuel Ray-Ikpe, amelielezea tukio hilo kama la bahati mbaya, la kushangaza na ajabu.

"Sijawahi kusikia kitu kama hicho kabla, lakini kimetokea kwetu, kanisani kwetu. Hatuna cha kufanya. Katibu wangu alikuja kutoka benki akilia. Mungu ndo anajua nini hasa kimetokea. Tumeyaacha yote kwenye mikono ya Mungu muumba wetu," alisema askofu huyo.
.

No comments:

Post a Comment