Sunday, May 13, 2012

Video haina hata wiki lakini ipo mtaani, nani kaifikisha?


Unapokutana mtaani na compilation ya video za Bongo iliyofanywa kienyeji na tena ikiwa na video mpya ambazo hazina hata wiki ama mwezi tangu zitoke unapatwa na swali gani?

Zimefikaje kwa ‘wezi’ hawa wa kazi za wasanii mapema hivi? Nani amewapa? Wamezitoa Youtube? Mbona zina quality sana tofauti na hizi zilizokuwa uploaded Youtube? 

Kwetu sisi jibu la haraka kabisa tunalolipata la jinsi video hizi zinavyowafikia wafanyabishara hawa ambao wengine mtaji wao ni computer moja iliyopo chumbani, ni kwamba wafanyakazi wa vituo vya TV ndio huzisambaza.

Ni ngumu kuzuia usambazaji huo wa video kutoka kwenye vituo vya TV kwenda mtaani, lakini kuna kauli yoyote ilishatoka kwa mamlaka husika husasan COSOTA kukemea hili? Kuna msaani yeyote alishawahi kuwakemea watu wa TV wasisambaze hovyo video zao? Hatujawahi kusikia. Ama wasanii wanapokutana na video hizi hubakia kujisifia kuwa wapo juu ndo maana ngoma zao zimo kwenye compilation hizo?



Ni wazi kuwa watu wa TV ndio wanaozisambaza video hizi na huenda miongoni mwao hujihusisha na kazi hii ya kurudufu video za wasanii na kuziuza mtaani.

Makala hii tumeiandika baada ya kukutana na compilation mbili za video za wasanii wa Bongo. Moja imepewa jina la ‘Videos Hot 2012’ yenye video 35! na nyingine ikiitwa ‘Bongo Collection yenye video 15.




















Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye Bongo Collection ni pamoja na Magubegube ya Barnaba, Nishike mkono ya C-Sir Madini, Samboira ya Ben Pol, Tabia gani ya Mr.Nice, Kamiligago ya Profesor J, Siri ya Penzi ya Shaa, Nimemuona ya Bright ft. Belle na nyingine nyingi mpya.



Piga picha msanii ndo ameanza. Amejichanga mpaka kafanya video nzuri. Hajaanza kupata hata shows za kufuta jasho lake lakini kuna mjanja mjini anaingiza hela tayari kwa kuuza video ya msanii huyu! Inauma.



Kama tumeshakubali kuwa video za Bongo Fleva ni kwa ajili ya promotion tu, mbona watu wa Gospel wanauza? Ama mbona hizo hizo zinazouzwa kinyemela zinanunuliwa kama njugu na nyingi zinatumiwa kuwaburudisha abiria kwenye mabasi ya mikoani au wateja kwenye baa ama vilabu vya pombe?








No comments:

Post a Comment