Friday, May 11, 2012

Sauti Sol kutumbuiza katika tamasha kubwa la barani Ulaya



Wanamuziki wa kundi la Sauti Sol la nchini Kenya wanatarajia kukwea pipa hadi Jamhuri ya Czech katika tamasha kubwa kabisa barani Ulaya liitwalo Colours of Ostrava.

Kundi hilo linaundwa na Bien-aime Baraza, Willis Austin Chimano, Delvin Mudigi na mpiga gitaa mkuu Polycarp Otieno.

Zaidi ya wasanii na bendi hamsini kubwa duniani watatumbuiza katika tamasha hilo akiwemo msanii wa Marekani Janelle Monae na nguli wa jazz barani Afrika Hugh Masekela.

Akiongea na mtandao wa penya-africa.com Chimano amesema Sauti Sol ambayo hupiga mahadhi ya Afro-pop itaenda kuonesha aina yao ya muziki yenye utofauti mkubwa.

Kwa upande wake Delvin anasema: “Tunataka kuuainisha muziki wa Africa. Sio sawa kabisa kwa wanamuziki wa Afrika kusahaulika. Ni mpango wetu kuuvunja mtazamo hasi uliopo kwasababu sisi ni rika jipya la muziki wa Afrika”

Kundi hilo limefanikiwa kushiriki mara nyingi kwenye matamasha ya kimataifa ambayo hayajawahi kuwa na wasanii kutoka Afrika Mashariki huku Polycarp akizungumzia siri ya mafanikio yao, “Sisi ni bendi ya kwanza kupenya kibaishara kwenye mkondo mkuu ambayo Kenya haijawahi kuwa nayo kwa kipindi kirefu”. 

Amesema kikubwa zaidi ni kuwa wao ni bendi ya kwanza ya Kenya/Afrika Mashariki kutumbuiza katika tamasha la SXSW (South by South West) ambalo mara ya mwisho limefanyika huko Austin, Texas.

“Ndoto yetu ni kupata mafanikio Africa na kimataifa” anasema Polycarp.

Kuhusu iwapo wakipata nafasi ya kukutana na Janelle Monae ambaye atatumbuiza pia kwenye tamasha hilo Bien amesema “ Hapana! lakini kama tukikutana naye, ntamwambia nimuoe! Natania!  Hakika lakini, yeye ni mtumbuizaji matata sana. Tutakuwa na mengi ya kusema na hatuwezi kuyasema yote sasa hivi. Nafasi ya kukutana naye itakuwa ni ndoto nyingine itakayotimia.

Janelle Monae
Tamasha hilo litafanyika kuanzia Alhamis ya 12 July 2012 — Jumapili 15 July 2012.

Uganda na Tanzania mko wapi?

No comments:

Post a Comment